

BINTI anayeshikilia Tuzo ya Mwigizaji
Bora wa Kike ya Ziff 2013, Elizabeth Michael maarufu Lulu ameweka wazi
kuwa amepata mchumba na kwamba taratibu za kujitambulisha na mahari
vitafuata baadaye.
“Unajua mimi ni binadamu na ili nitulie
na kujiepusha na majanga, ni vyema kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu,
anayenijali mimi na kazi yangu hapo nitasimama na kusema kwamba nimepata
sehemu ya kutulia na kuanza maisha mapya ya uhusiano na ndoa,” anasema
Lulu.
Hata hivyo anasema yeye na mchumba huyo
(ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake) wana mikakati mingi katika
kuyafikia maisha ya uhusiano yaliyo wazi na yenye baraka za wazazi.
“Siwezi kukutajia jina kwa sasa itafika
wakati atajulikana tu, hata hivyo bado hatujafikia hatua muhimu ikiwa ni
pamoja na kujitambulisha kwa wazazi na masuala ya mahari na ndoa. Vitu
kama hivi vitafanyika baadaye mwaka huu, hata hivyo wazazi wangu sidhani
kama watakuwa na pingamizi katika hili kwani mimi ni mtoto wa kike na
nimekua sasa,” anasema.
Kuhusu Mama Kanumba Lulu anasema: “Huyu
ni mama yangu hana tofauti na mama Lulu hivyo anajua kila kitu na
amenipa baraka zake zote, yaliyopita si ndwele kinachotakiwa ni kuganga
yajayo, namshukuru mama kwani amenionyesha upendo wa kweli na kunishauri
katika maisha, bila yeye nisingekuwa na ujasiri nilionao sasa.
“Mama Kanumba ni rafiki yangu wa ukweli,
ana mapenzi mazito sana kwangu amekuwa mstari wa mbele kunishauri na
kunipa mwongozo wa maisha ni nini na wapi nilipokosea na natakiwa
kufanya nini ili kuwa na maisha yaliyonyooka,” anasema mwigizaji huyo
anayetamba na filamu ya Foolish Age.
Lulu mwenye miaka 19, anasema haikuwa
rahisi kwake kufikiria kutulia kiuhusiano ila amepewa mwongozo bora
unaomfanya afikirie kufanya hivyo kwa sasa.
“Mimi ni binti na kama ujuavyo nina
mapenzi yangu moyoni, si kazi rahisi kuamua kwa sasa lakini nimepewa
mwongozo bora na kuona nini natakiwa kufanya. Kama binti napaswa
kuzingatia maadili, mimi ni kioo cha jamii, inafika hatua inabidi niishi
katika maadili hilo ndilo ninalolifanya sasa.”
Anasema wazazi wake wamempa baraka zote
kuhusu uhusiano wake wa sasa: “Wazazi wangu sasa wanafahamu kwamba
nimepata mchumba, kwa kweli wamenipa baraka zao zote, pande zote hata
Mama Kanumba. Nimekua sasa na mimi nina uamuzi wangu, ni vema kuangalia
ninataka nini lakini kikubwa wananishauri.”
Anasema wazazi wake hawakubali kila
anachokitaka: “Sina wazazi wa kukubali kila ninachokitaka ila nina
wazazi waelewa, wenye kuangalia jambo kabla hawajaniambia sasa unaweza
kuendelea, mama yangu ni mkali sana, hana mchezo hasa pale anapoona
kwamba nayumba kimaisha,” anasema Lulu.
Kuhusu tetesi zilizoenea kwamba ana
uhusiano na msanii wa hip hop Young Dee, Lulu alikana na kusisitiza
kwamba hajawahi hata kuwa na ukaribu na msanii huyo.
“Nashangaa taarifa hizo watu wanazitoa
wapi na mpaka leo nashangazwa na uvumi ulioenea kwamba tulifumaniwa,
usiku ule nilikuwa sehemu nyingine tofauti kabisa, ukweli ni kwamba
sijawahi kuwa na ukaribu na Young Dee, wala hata kumfikiria kama
ninaweza kuwa na uhusiano naye. Bado, hatulingani kwa kweli,” anasema.
0 comments:
Chapisha Maoni